26 days ago
UDSM YABUNI TEKNOLOJIA YA UFUGAJI SAMAKI INAYOTUMIA MAJI KIDOGO NA ENEO DOGO
Na Asha Mwakyonde, DODOMA
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),kimeonesha teknolojia mpya ya ufugaji wa samaki inayolenga kuongeza tija kwa wafugaji kwa kutumia maji kidogo na eneo dogo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza uchumi wa buluu nchini.
Akizungumza leo Agosti 3, 2026 katika banda la Chuo hicho kwenye Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea Dodoma, Mhadhiri Msaidizi kutoka Shule ya Sayansi Asilia na Teknolojia ya Uvuvi ya UDSM, Ndalo Missana amesema teknolojia hiyo inamwezesha mfugaji kufuga samaki huku maji yakisafishwa na kutumika tena, hatua inayopunguza gharama za uzalishaji.
Amesema ubunifu huo unalenga kuwasaidia wafugaji wadogo na wakubwa kuongeza uzalishaji wa samaki bila kuhitaji maeneo makubwa ya ufugaji.
"Tumekuja na teknolojia ya ufugaji wa samaki inayotumia maji kidogo lakini pia eneo dogo. Ni ubunifu unaomwezesha mfugaji kufuga samaki huku maji yakiendelea kusafishwa na hivyo kuongeza uzalishaji na kipato katika sekta ya uchumi wa buluu," amesema Missana.
Ameongeza kuwa mbali na teknolojia hiyo, chuo hicho pia kimebuni mfumo mwingine wa ufugaji unaohamishika ambao unaweza kuwekwa sehemu mbalimbali kulingana na mahitaji ya mfugaji na una uwezo wa kuhifadhi samaki wengi kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa Missana, UDSM pia inazalisha mbegu bora za samaki pamoja na chakula bora cha samaki ambacho kinawafikia wafugaji ili kuwawezesha kupata matokeo mazuri katika ufugaji wao.
Amesema teknolojia hizo zinaendana na azma ya Serikali ya kuongeza uzalishaji wa samaki na kufikia malengo ya kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa Taifa.
"Tunazalisha mbegu bora na chakula bora cha samaki ili kuhakikisha wafugaji wetu wanafuga kwa tija na kuongeza kipato chao," amesema.
Akizungumzia namna ya kuwafikia wafugaji wanaohitaji teknolojia hizo, Missana amesema UDSM imekuwa ikitumia majukwaa mbalimbali ikiwemo maonesho ya Nane Nane, Sabasaba pamoja na maonesho yanayoandaliwa na chuo hicho kutoa elimu na mawasiliano kwa wananchi.
Amesema wafugaji wanaweza pia kuwasiliana moja kwa moja na chuo ili kupata mafunzo au msaada wa kitaalamu katika kutumia teknolojia hizo kwenye maeneo yao.
Aidha, amesema ubunifu huo umehusisha pia wanafunzi wa UDSM ambao wamepata fursa ya kujifunza kwa vitendo na kushiriki katika tafiti zinazolenga kutatua changamoto za wafugaji.
Ameeleza kuwa teknolojia hiyo ina manufaa kwa pande zote, ikiwemo wabunifu kupata uzoefu wa kitaaluma, wanafunzi kupata ujuzi na jamii kunufaika kupitia njia rahisi za kuongeza uzalishaji wa samaki.
"Mchango wake ni mkubwa kwa sababu tunaona watu wanakuja kujifunza teknolojia hizi. Lengo ni kuhakikisha wafugaji wanatumia teknolojia zinazoongeza tija na kuboresha ufugaji wao," amesema Missana.
Read article